Wednesday, February 11, 2015

JIHAD YA NDOA

UZITO WA NDOA KWA DUNIA YA SASA


Imekuwa jambo gumu sana kwa vijana kufikiria kuoa hasa kwa kipindi hiki kizito kiiman kwa sasa
Ni hali a kawaida kabisa kwa kijana wa kisasa kumkuta yupo katika hali nzuri ya kujikim kwa kila kitu lakini asitimize ibada hii ya ndoa
kurasa hii nataka nielezee umuhimu wa ndoa katika uislamu

FAIDA ZA NDOA
Mwenyezi Mungu Sub-hana huwataala anasema katika Qur'an

"Qur’an 30:21

Na katika lama zake amewaumbieni wake kutokana na nyinyi wenyewe ili muishi kwa utulivu nao, na akawatia upendo na rehema kati ya nyoyo zenu. Kwa hakika katika haya ni ishara kwa wenye kufikiri.

 

Qur’an 16:72

Na Allah amekuumbieni anaetokana na asili yenu na kwa ajili yenu, kutoka

kwao watoto wa kiume na wakike na wajukuu na kuwapeni rizki njema”. "

Na katika maneno yake Mtume Muhammad (S.A.W)

Enyi vijana, aliye na uwezo wa kuoa aoe, kufanya hivyo kutamsaidia kuinamisha macho yake chini na kuwa mtii. Na utii ni sehemu ya imani”. (Bukhari).


Na katika hadithi nyingine pia amesema:

“Ndoa ni katika mienendo yangu na atakayekwenda kinyume na hivyo hatakuwa nami” (Bukhari).


Kwa ufupi ndoa katika uislamu ni:

1.    Njia mojawapo ya ibada. Mnapokuwa katika ndoa mnakuwa mpo katika kumuabudu Mwenyezi Mungu na kufuata mwenendo wa mtume wake.

2.    Kujenga uhusiano wa familia na makundi (jamii).

3.    Ni kitendo cha uchaji Mungu.

4.    Njia halali ya kuzaliana.

5.    Mojawapo ya suluhisho la kuondoa kuchanganyikiwa.

 

JE NDOA NI LAZIMA?

Imamu Abu Hanifa, Ahmadbin Hanbal na Malik wanasema ingawa asili yake inaonekana ni jambo lisilokuwa la laima lakini kwa baadhi ya watu linakuwa ni lazima (wajibu).

 

Imamu Shaafi anasema ni jambo lenye kupendeza (Mubah).

 

Imeripotiwa na bukhari na wengineo kwamba watu watatu walienda kwa wake za mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) na kuwauliza vipi mtume afanyavyo ibada zake. Walivyoelezwa wakaona inabidi wao eafanye zaidi ya vile alivyokuwa akifanya mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) kwa kuona kuwa kunatofauti kubwa sana kati yao na mtume kiibada japo yeye ni mtu ambaye amesamehewa madhambi yake yote ya nyuma na ya mbeleni. Mmoja wao akasema ataswali usiku daima. Mwingine akasema hatoshughulika na habari za wanawake na hivyo hatooa. Na wa mwisho akasema atafunga daima. Mtume aliposikia habari zao akasema:

 

“Mimi ni mcha Mungu zaidi yenu, pamoja na hayo ninafunga na kufungua, nina sali na kulala na nina oa. Yule atakaye kwenda kinyume hatakuwa pamoja nami”.

 

Wanachuoni wamefikia makubaliano kuwa ndoa ni lazima kwa muislamu mwenye uwezo wa kumuhudumia mke. Allah ameahidi kuwasaidia wale wenye kuoa kwaajili ya kujikinga pale aliposema:

“Waozesheni miongoni mwenu wale walio wajane na wema miongoni mwa wajakazi wenu waume au wake iwapo masikini, Allah atawatajirisha kutokana na hazina zake”. (24:32).

 

Mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) amesema:

“Kuna aina tatu za wenye haki ya msaada wa Allah, mwenye kuoa kutaka aishi maisha mema, mtumwa ambae bwana wake amekubali kununua uhuru wake atakapo kuwa tayari kulipa na mwenye kupigana katika njia ya Allah”. (Ahmad, An-Nisai, Attirmidhiy, Ibn Majah na al-Hakim).

 

WANAWAKE WASIO RUHUSIWA KUWAOA

 

1-    Mke wa baba, awe ameachwa au kafiliwa na baba.

2-    Mama, wakiwemo mabibi wa pande zote.

3-    Binti, wakiwemo wajukuu wa kike kutokana na watoto wako wa kike au wa kiume.

4-    Dada, akiwemo wa baba au mama mmoja.

5-    Shangazi kwa baba, au mama mmoja na baba.

6-    Binti wa kaka.

7-    Binti wa dada.

8-    Mama aliyekunyonyesha.

9-    Mabinti wa mama aliyekunyonyesha.

10- Mkwe wako wa kike (mama wa mke).

11- Ndugu wawili wa kike kuwaoa wakati mmoja.

12- Mwanamke mshirikina (anayeabudu masanamu).

13- Kahaba

Inaelezwa kuwa Murtaid ibn Murtaid alimuomba Mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) amuoe mwanamke aitwae Anaq ambae alikuwa na uhusiano naye kabla ya uislam. Mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) hakumjibu mpaka aya ikashuka isemayo:

“Mzinifu mwanamume hatooa ila mzinifu mwanamke au mshirikina mwanamke na mzinifu mwanamke hatoolewa na yoyote ila na mzinifu mwanamume au mshirikina mwanaume. Na kuwaoa hawa ni haramu kwa muumini.”

Mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) akamsomea Murtaid hiyo aya na kumwambia asimuoe (Abu Daaud, an-Nisai na Tirmidhiy).


KUCHUMBIA


-       Hairuhusiwi kumposa mwanamke alie katika eda ya kuachwa au kufiwa na mume kwani wakati huu huhesabiwa ni sehemu ya ndoa yake mwanamke.

-       Hairuhusiwi kumposa mwanamke ambaye anajulikana kuwa amekwishaposwa na mtu mwingine.

Katika hadithi iliyopokelewa na Muslim, Mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) anasema:

“Muumini ni ndugu wa muumini mwingine. Kwa hivyo hairuhusiwi kwake kumpiku ndugu yake katika kununua kitu au kutoa posa kwa mwanamke wakati anapokuwa ndugu yake ameshaposa, ila awe amempa ruhusa”.

 

KUMUONA MCHUMBA UNAETAKA KUMUOA

Ina ruhusiwa kumuona mchumba kwa sababu wanaosema jicho ni mtumishi wa moyo. Na macho yatakapoonana na kukutana na nyoyo za mume na mke zinaweza zikakutana.

Al-Mughirah ibn Shui’bah amesema:

“Nilitaka kumuoa mwanamke, mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) akaniuliza kama nimemwangalia nikamjibu bado akaniambia nikamwangalie kwani kufanya hivyo kunaweza kuleta mapenzi kati yetu. Nikaenda kwa wazazi wake na kuwajulisha ushauri wa mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) wakawa wamesita juu ya hilo. Binti yao akasikia maongezi akasema: ‘iwapo mtume amesema uniangalie basi niangalie’. Nikamwangalia na hatimae nikamuoa”. (Ahmad, al-Tilmidh, ibn Majah, ibn Hakim).

NIKAHA

Mambo yatakikanayo kutimia ili ndoa ikamilike kufungwa.

1.    Mlezi: Baba au mwakilishi wake wa kutoa idhini.

2.    Mahari (Qur’an 4:4):

“Wapeni wanawake mahari yao…”.

3.    Muoaji na Muolewaji.

4.    Kauli ya kuozesha na kukubali.

5.    Mashahidi wawili.

MAISHA YA NDOA

Qur’an (2:187):

            “Wao ni vazi kwenu nanyi ni vazi kwao”.

Ikimaananisha ulinzi kwa kila mmoja wenu kujikinga kwa mwenzie, kupeana msaada na kila mmoja ana haki kwa mwingine.

Qur’an (2:228):

“… na wao wanawake wana haki sawa na wanaume juu yao kwa heshima, ila wanaume wamewazidi kwa kiasi”.

Huku kuzidi hutokana na jukumu la mume kuwa ni kiongozi wa familia.

Mtume aliulizwa na mtu “Ewe mjumbe wa Mwenyezi Mungu. Ni haki zipi awezazo kuzitaka mke kwa mumewe?”

Akajibu:

“Umlishe kama ujilishavyo, umvishe kama ujivishavyo, usimpige katu usoni kwake au kumfanya duni au kujiepusha nae ila iwe ndani ya nyumba”. (Abu Daaud na Ibn Hibaan).

 

Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam amesema kuhusu haki ya mume:

Hairuhusiwi kwa mwanamke anayeamini Allah kumruhusu yeyote kwenye nyumba ya mumewe iwapo mume hapendi. Asitoke nje ya nyumba kama hapendi. Na asimsikilize yeyote anayepingana na amri zake. Asikatae kushirikiana kitanda, asimpige iwapo ana nguvu”. (Al-Hakim).

 

Qur’an (4:19)

“Na pataneni nao kwa upole iwapo mnawachukia, inawezekana mkachukia kitu ambacho Allah amekiwekea uzuri mwingi”.

 

TALAKA

Amesema Mtume:

“Miongoni mwa vitu halali, talaka ni kitu kinacho chukiwa zaidi na Allah”

. (Abu Daaud).

 

Inapofikia njia zote zaupatanishi zimeshindikana, uislamu unaruhusu kuachana.

Qur’an (4:130)

            “Lakini watakapoachana, Allah atawapa kila mmoja hazina zake…”.

Hairuhusiwi kutoa talaka wakati mke yupo kwenye hedhi au baada ya kujifungua au akiwa mjamzito na mume anajua.

Sababu ya kukataza talaka kutolewa mwanamke akiwa na hedhi na baada ya kujifungua ni kwamba hairuhusiwi kumuingilia mwanamke wakati wa hali hizo.

Abdallah ibn Umar alimwacha mke wake akiwa na hedhi. Umar (RA) alimweleza mtume jambo hili akasema: “Amrejee. Iwapo anataka kumwacha afanye hivyo baada ya tohara kabla ya tendo la ndoa, huo ndio wakati wa kusubiri ambao Allah (Subhaanahu Wata’ala) ameutoa kwa kuacha”.

Qur’an (65:1):

            “Ewe Mtume, uachapo mke mwache katika muda maalum uliowekwa”.

Je ukimwacha katika moja ya vipindi hivyo hapo juu, talaka inakuwa ni halali?

Ndiyo inakuwa ni halali. Lakini mume atakuwa ni mwenye madhambi.

Baada ya kuachwa mke anatakiwa kubaki ndani ya nyumba ya mumewe kwa kipindi cha eda yake. Hii inatoa nafasi ya kuweza kurejeana ikiwa hii ni talaka ya kwanza au ya pili.

Qur’an (65:1):

(Na Muogopeni Allah mola wenu. Msiwaondoe nje ya nyumba zao, nao hawapaswi kuondoka ila iwapo watafanya kitendo kiovu, na hii ndio mipaka iliyowekwa na Allah. Na yeyote atakae ivuka mipaka ya Allah, hakika anaikosea nafsi yake”.

Hivyo watakapoachana na waachane kwa wema bila matusi wa ugomvi na kuvunjiana heshima.

Qur’an (65:2) “ Kaeni kwa wema au achaneni kwa wema”.

            (2: 229) “Halafu baki nae kwa heshima au mwache kwa heshima”.


HAKI YA MKE KUDAI TALAKA

Mke nae ana haki ya kudai talaka, kama ilivyo katika Qur’an:

“Na iwapo nyinyi (makadhi) mnahofia kwamba hao wawili hawataweza kuchunga mipaka ya Allah iliyowekwa, hakuna lawama kwa yeyote kati yao, iwapo atataka mke kujiepusha na ndoa akirudisha mahari yote au sehemu yake”.


 

0 comments:

Post a Comment

MWEZI WA MUHARRAAM NA UZUSHI

بسم الله الرحمن الرحيم MASHIA NA BIDAA ZA MWEZI WA MUHARRAMU. Mwezi wa Muharramu ni miongoni mwa miezi mitukufu kwa mujibu wa mafundis...