Wednesday, February 11, 2015

JIHAD YA NDOA

UZITO WA NDOA KWA DUNIA YA SASA


Imekuwa jambo gumu sana kwa vijana kufikiria kuoa hasa kwa kipindi hiki kizito kiiman kwa sasa
Ni hali a kawaida kabisa kwa kijana wa kisasa kumkuta yupo katika hali nzuri ya kujikim kwa kila kitu lakini asitimize ibada hii ya ndoa
kurasa hii nataka nielezee umuhimu wa ndoa katika uislamu

FAIDA ZA NDOA
Mwenyezi Mungu Sub-hana huwataala anasema katika Qur'an

"Qur’an 30:21

Na katika lama zake amewaumbieni wake kutokana na nyinyi wenyewe ili muishi kwa utulivu nao, na akawatia upendo na rehema kati ya nyoyo zenu. Kwa hakika katika haya ni ishara kwa wenye kufikiri.

 

Qur’an 16:72

Na Allah amekuumbieni anaetokana na asili yenu na kwa ajili yenu, kutoka

kwao watoto wa kiume na wakike na wajukuu na kuwapeni rizki njema”. "

Na katika maneno yake Mtume Muhammad (S.A.W)

Enyi vijana, aliye na uwezo wa kuoa aoe, kufanya hivyo kutamsaidia kuinamisha macho yake chini na kuwa mtii. Na utii ni sehemu ya imani”. (Bukhari).


Na katika hadithi nyingine pia amesema:

“Ndoa ni katika mienendo yangu na atakayekwenda kinyume na hivyo hatakuwa nami” (Bukhari).


Kwa ufupi ndoa katika uislamu ni:

1.    Njia mojawapo ya ibada. Mnapokuwa katika ndoa mnakuwa mpo katika kumuabudu Mwenyezi Mungu na kufuata mwenendo wa mtume wake.

2.    Kujenga uhusiano wa familia na makundi (jamii).

3.    Ni kitendo cha uchaji Mungu.

4.    Njia halali ya kuzaliana.

5.    Mojawapo ya suluhisho la kuondoa kuchanganyikiwa.

 

JE NDOA NI LAZIMA?

Imamu Abu Hanifa, Ahmadbin Hanbal na Malik wanasema ingawa asili yake inaonekana ni jambo lisilokuwa la laima lakini kwa baadhi ya watu linakuwa ni lazima (wajibu).

 

Imamu Shaafi anasema ni jambo lenye kupendeza (Mubah).

 

Imeripotiwa na bukhari na wengineo kwamba watu watatu walienda kwa wake za mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) na kuwauliza vipi mtume afanyavyo ibada zake. Walivyoelezwa wakaona inabidi wao eafanye zaidi ya vile alivyokuwa akifanya mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) kwa kuona kuwa kunatofauti kubwa sana kati yao na mtume kiibada japo yeye ni mtu ambaye amesamehewa madhambi yake yote ya nyuma na ya mbeleni. Mmoja wao akasema ataswali usiku daima. Mwingine akasema hatoshughulika na habari za wanawake na hivyo hatooa. Na wa mwisho akasema atafunga daima. Mtume aliposikia habari zao akasema:

 

“Mimi ni mcha Mungu zaidi yenu, pamoja na hayo ninafunga na kufungua, nina sali na kulala na nina oa. Yule atakaye kwenda kinyume hatakuwa pamoja nami”.

 

Wanachuoni wamefikia makubaliano kuwa ndoa ni lazima kwa muislamu mwenye uwezo wa kumuhudumia mke. Allah ameahidi kuwasaidia wale wenye kuoa kwaajili ya kujikinga pale aliposema:

“Waozesheni miongoni mwenu wale walio wajane na wema miongoni mwa wajakazi wenu waume au wake iwapo masikini, Allah atawatajirisha kutokana na hazina zake”. (24:32).

 

Mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) amesema:

“Kuna aina tatu za wenye haki ya msaada wa Allah, mwenye kuoa kutaka aishi maisha mema, mtumwa ambae bwana wake amekubali kununua uhuru wake atakapo kuwa tayari kulipa na mwenye kupigana katika njia ya Allah”. (Ahmad, An-Nisai, Attirmidhiy, Ibn Majah na al-Hakim).

 

WANAWAKE WASIO RUHUSIWA KUWAOA

 

1-    Mke wa baba, awe ameachwa au kafiliwa na baba.

2-    Mama, wakiwemo mabibi wa pande zote.

3-    Binti, wakiwemo wajukuu wa kike kutokana na watoto wako wa kike au wa kiume.

4-    Dada, akiwemo wa baba au mama mmoja.

5-    Shangazi kwa baba, au mama mmoja na baba.

6-    Binti wa kaka.

7-    Binti wa dada.

8-    Mama aliyekunyonyesha.

9-    Mabinti wa mama aliyekunyonyesha.

10- Mkwe wako wa kike (mama wa mke).

11- Ndugu wawili wa kike kuwaoa wakati mmoja.

12- Mwanamke mshirikina (anayeabudu masanamu).

13- Kahaba

Inaelezwa kuwa Murtaid ibn Murtaid alimuomba Mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) amuoe mwanamke aitwae Anaq ambae alikuwa na uhusiano naye kabla ya uislam. Mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) hakumjibu mpaka aya ikashuka isemayo:

“Mzinifu mwanamume hatooa ila mzinifu mwanamke au mshirikina mwanamke na mzinifu mwanamke hatoolewa na yoyote ila na mzinifu mwanamume au mshirikina mwanaume. Na kuwaoa hawa ni haramu kwa muumini.”

Mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) akamsomea Murtaid hiyo aya na kumwambia asimuoe (Abu Daaud, an-Nisai na Tirmidhiy).


KUCHUMBIA


-       Hairuhusiwi kumposa mwanamke alie katika eda ya kuachwa au kufiwa na mume kwani wakati huu huhesabiwa ni sehemu ya ndoa yake mwanamke.

-       Hairuhusiwi kumposa mwanamke ambaye anajulikana kuwa amekwishaposwa na mtu mwingine.

Katika hadithi iliyopokelewa na Muslim, Mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) anasema:

“Muumini ni ndugu wa muumini mwingine. Kwa hivyo hairuhusiwi kwake kumpiku ndugu yake katika kununua kitu au kutoa posa kwa mwanamke wakati anapokuwa ndugu yake ameshaposa, ila awe amempa ruhusa”.

 

KUMUONA MCHUMBA UNAETAKA KUMUOA

Ina ruhusiwa kumuona mchumba kwa sababu wanaosema jicho ni mtumishi wa moyo. Na macho yatakapoonana na kukutana na nyoyo za mume na mke zinaweza zikakutana.

Al-Mughirah ibn Shui’bah amesema:

“Nilitaka kumuoa mwanamke, mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) akaniuliza kama nimemwangalia nikamjibu bado akaniambia nikamwangalie kwani kufanya hivyo kunaweza kuleta mapenzi kati yetu. Nikaenda kwa wazazi wake na kuwajulisha ushauri wa mtume (Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam) wakawa wamesita juu ya hilo. Binti yao akasikia maongezi akasema: ‘iwapo mtume amesema uniangalie basi niangalie’. Nikamwangalia na hatimae nikamuoa”. (Ahmad, al-Tilmidh, ibn Majah, ibn Hakim).

NIKAHA

Mambo yatakikanayo kutimia ili ndoa ikamilike kufungwa.

1.    Mlezi: Baba au mwakilishi wake wa kutoa idhini.

2.    Mahari (Qur’an 4:4):

“Wapeni wanawake mahari yao…”.

3.    Muoaji na Muolewaji.

4.    Kauli ya kuozesha na kukubali.

5.    Mashahidi wawili.

MAISHA YA NDOA

Qur’an (2:187):

            “Wao ni vazi kwenu nanyi ni vazi kwao”.

Ikimaananisha ulinzi kwa kila mmoja wenu kujikinga kwa mwenzie, kupeana msaada na kila mmoja ana haki kwa mwingine.

Qur’an (2:228):

“… na wao wanawake wana haki sawa na wanaume juu yao kwa heshima, ila wanaume wamewazidi kwa kiasi”.

Huku kuzidi hutokana na jukumu la mume kuwa ni kiongozi wa familia.

Mtume aliulizwa na mtu “Ewe mjumbe wa Mwenyezi Mungu. Ni haki zipi awezazo kuzitaka mke kwa mumewe?”

Akajibu:

“Umlishe kama ujilishavyo, umvishe kama ujivishavyo, usimpige katu usoni kwake au kumfanya duni au kujiepusha nae ila iwe ndani ya nyumba”. (Abu Daaud na Ibn Hibaan).

 

Mtume Salla Allahu ‘Alayhi Wasallam amesema kuhusu haki ya mume:

Hairuhusiwi kwa mwanamke anayeamini Allah kumruhusu yeyote kwenye nyumba ya mumewe iwapo mume hapendi. Asitoke nje ya nyumba kama hapendi. Na asimsikilize yeyote anayepingana na amri zake. Asikatae kushirikiana kitanda, asimpige iwapo ana nguvu”. (Al-Hakim).

 

Qur’an (4:19)

“Na pataneni nao kwa upole iwapo mnawachukia, inawezekana mkachukia kitu ambacho Allah amekiwekea uzuri mwingi”.

 

TALAKA

Amesema Mtume:

“Miongoni mwa vitu halali, talaka ni kitu kinacho chukiwa zaidi na Allah”

. (Abu Daaud).

 

Inapofikia njia zote zaupatanishi zimeshindikana, uislamu unaruhusu kuachana.

Qur’an (4:130)

            “Lakini watakapoachana, Allah atawapa kila mmoja hazina zake…”.

Hairuhusiwi kutoa talaka wakati mke yupo kwenye hedhi au baada ya kujifungua au akiwa mjamzito na mume anajua.

Sababu ya kukataza talaka kutolewa mwanamke akiwa na hedhi na baada ya kujifungua ni kwamba hairuhusiwi kumuingilia mwanamke wakati wa hali hizo.

Abdallah ibn Umar alimwacha mke wake akiwa na hedhi. Umar (RA) alimweleza mtume jambo hili akasema: “Amrejee. Iwapo anataka kumwacha afanye hivyo baada ya tohara kabla ya tendo la ndoa, huo ndio wakati wa kusubiri ambao Allah (Subhaanahu Wata’ala) ameutoa kwa kuacha”.

Qur’an (65:1):

            “Ewe Mtume, uachapo mke mwache katika muda maalum uliowekwa”.

Je ukimwacha katika moja ya vipindi hivyo hapo juu, talaka inakuwa ni halali?

Ndiyo inakuwa ni halali. Lakini mume atakuwa ni mwenye madhambi.

Baada ya kuachwa mke anatakiwa kubaki ndani ya nyumba ya mumewe kwa kipindi cha eda yake. Hii inatoa nafasi ya kuweza kurejeana ikiwa hii ni talaka ya kwanza au ya pili.

Qur’an (65:1):

(Na Muogopeni Allah mola wenu. Msiwaondoe nje ya nyumba zao, nao hawapaswi kuondoka ila iwapo watafanya kitendo kiovu, na hii ndio mipaka iliyowekwa na Allah. Na yeyote atakae ivuka mipaka ya Allah, hakika anaikosea nafsi yake”.

Hivyo watakapoachana na waachane kwa wema bila matusi wa ugomvi na kuvunjiana heshima.

Qur’an (65:2) “ Kaeni kwa wema au achaneni kwa wema”.

            (2: 229) “Halafu baki nae kwa heshima au mwache kwa heshima”.


HAKI YA MKE KUDAI TALAKA

Mke nae ana haki ya kudai talaka, kama ilivyo katika Qur’an:

“Na iwapo nyinyi (makadhi) mnahofia kwamba hao wawili hawataweza kuchunga mipaka ya Allah iliyowekwa, hakuna lawama kwa yeyote kati yao, iwapo atataka mke kujiepusha na ndoa akirudisha mahari yote au sehemu yake”.


 

Tuesday, February 10, 2015

SIKUKUU ZA KIDINI

ACHA YASIYOKUHUSU




Katika uislamu zimeidhinishwa sikukuu tatu tu

  1. Idd al hajj
  2. Idd al fitri
  3. Aljumaaa.
Tofauti na hizo acha kusherehekea muislam

JIHAD YA NAFSI

MAPAMBANO DHIDI YA NAFSI YAKO

Roho ya binadamu ni eneo la mapambano ya nguvu mbili za mashindano. Nguvu ya Mungu humvutia mtu kwenye nyanja ya mbinguni, na kumhamasisha kwenye matendo ya wema. Nguvu za kishetani humshawishi kuelekea maeneo ya giza na aibu, na kumualika kwenye matendo maovu. Wakati nguvu ya Mungu ni ushindi, mtu anaibuka kuwa mwema na mpole, kwenye ufuasi wa Mtume (S), watu wa Mungu, na wacha Mungu. Wakati, hata hivyo, vikosi vya kishetani hutawala, mtu anakuwa muasi na muovu na kuwa katika kundi pamoja na makafiri, madhalimu, watenda maovu na wale ambao wamelaaniwa.

""Na kwa nafsi na kuilinganisha kwake! Akaifahamisha uovuna takua yake. Hakika amefaulu aliyeitakasa (Qur'an, 91: 7-9)""

MANENO YA MTUME(S.A.W)

""Imam Ja'far al-Sadiq (as) amesema: "Mtume wa Mwenyezi Mungu Muhammad(s) alipeleka kikosi cha jeshi (kwenye uwanja wa mapambano). Walipata ushindi wakati waliporudi kwao, yeye Mtume (s) alisema: '. Heri yao wale ambao walifanya jihadi ndogo na bado kufanya jihadi kubwa' Wakati alipoulizwa, 'Ni ipi Jihad kubwa? Mtume (s.a.w.w) akasema : 'jihadi ya nafsi (mapambano dhidi ya wewe mwenyewe)' ".[Al-Majlisi, Bihar al-Anwar, Juzuu ya 19, uk. 182, hadith namba. 31]""

USHAURI KATIKA MAPAMBANO YA NAFSI YAKO
  1. Ni asili ya binadamu kumshukuru mwingine ambaye amekuwa mwema.Tafakari na kadiria zile fadhila za dhahiri na za siri alizotupa Mwenyezi juu yetu.Viumbe wote wa Mungu hawawezi hata kutoa sehemu ya fadhila hizo.

  2. Angalia hewa tunayopumua sisi mchana na usiku, na juu ya maisha yetu ambayo pia ile ya viumbe hai wengine ni tegemezi. Hakuna kinachoweza kubakia hai kama kikinyimwa hewa hata kwa dakika chache. Ni vipi zawadi hii ya ajabu ya Mungu! Kama watu wote wa ulimwengu wataungana pamoja kwa kazi hii, hawataweza kuunda zawadi hii, hawataweza kufanya hivyo. Katika njia hiyo hiyo, tafakari juu ya karama zingine za Mungu kama vile hisia za nje za mwili za kuona, kusikia, ladha, harufu, na kugusa, na uwezo wa ndani kama vile kufikiri, dhana, na kuhoji, kila mmoja ambaye amebeba faida zisizo na ukomo na ambazo zimetolewa kwetu na Bwana wetu. Mwenyezi Mungu Muumba na Mfalme wa ulimwengu huu. Binadamu, ni kiumbe aliyewekwa katika moja ya sayari ndogo, ameshindwa kabisa kufahamu kiwango kidogo cha dunia yake mwenyewe, jua ambalo hawezi hata kulilinganisha na sayari nyingine ya jua iliyoko mbali zaidi ya kundi la nyota. Mfumo wetu wa jua ni kitu kisicholinganishwa na mifumo kadhaa ya nishati ya jua, ambayo bado haijaepuka darubini yenye nguvu kubwa ya wapelelezi na wachunguzi. Angalia katika ubongo wa binadamu-ni kipi wanachovutia viumbe! Je, yawezekana binadamu kuunganisha jitihada zao na kuweza kufanya hata moja seli hai ya ubongo (kiini cha ubongo) ambayo Mwenyezi Mungu ameumba na ameiumba kwa wakati wote! Hakika hii akili tuliyopewa na Mungu inastahili kuwa kiti cha mawazo na maongozi mema tu, na wala sio mawazo mabaya!   ALLAH AALAM


Sunday, February 8, 2015

USIJIANDAE KWA RANGI NYEKUNDU YA VALENTINE



KUJITOA MUHANGA NA UISLAMU

'"

Na wale wanaowaudhi Waumini wanaume na wanawake pasina wao kufanya kosa lolote, bila ya shaka wamebeba dhulma kubwa na dhambi zilizo dhahiri

""
((Damu ya Muislamu haipasi kumwagwa isipokuwa katika hali tatu:  Mzinzi Muolewa (Mtu  mzima aliyeoa/olewa), uhai kwa uhai (nafsi kwa nafsi) na kwa yule anaeeacha dini  na akajifarikisha na  jama’ah (kundi) (amejitenga na watu wa dini yake)) [Imesimuliwa na Al-Bukhaariy na Muslim]

""

Nimetanguliza hadithi hizo mbili kuonesha jinsi gani uislamu unapinga muislamu kumuua muislamu mwenzake.
KUJITOA MUHANGA NI NINI ??

Ni hali ya mtu mmoja kujiwekea mazingira yake kama mtego wa kuua kundi la watu kwa katika mazingira ya kujilipua  akiwa amevaa mabomu au kipando chake kikiwa kimefungwa na mabomu.
Hali kama hii haijalishi kwenye kundi lengwa la watu (Target required) kuna muislamu,watoto,au wanawake ambao katika uislamu imekatazwa kuwadhulu endapo mpo katika viwanja vya vita.sasa iweje imani hii ya muhanga wa mabomu iwekwe katika uislamu ??
Utagundua kuna sababu zilizojificha za kujitolea muhanga ili kuuangamiza uislamu na lengo hasa la uislamu kwa vizazi changa vijavyo.
Maana halisi ya uislam ni salama na amani.
Hakuna hali yoyote ya kupigania uislamu kwa kujitoa uhai wako hali ya kuwa adui huyo wa uislamu yupo hai .kwa maana mabomu umejifunga wewe jee kama yatalipuka bila muhusika kufa utakuwa umeupigania uislamu ?? jibu moja kwa moja ni hapana.
Muislamu kumuua muislam mwenzake iwe kwa bahati mbaya ama kwa kukusudia imetengewa toba na Mwenyez MUNGU sub-hana hu wataala(Allah).kwa maana si ruhusa kwa hilo jambo,jee hatuoni kwenye muhanga  waislam wanauawa ??
Tafakali na jifunze kwa hayo   ALLAH AALAM

'"

Saturday, February 7, 2015

IJUE JIHHAD YA KWELI KATIKA UISLAMU


JIHADI ni neno lililopotoshwa maana yake kwa makusudi. Leo neno hilo limepoteza kabisa ile maana yake halisi. Maana ya jihadi imegeuzwa kuwa ni vita, umwagaji damu na ulipuaji mabomu! Hilo halikutokea kwa bahati mbaya. Ni mkakati maalumu ulioandaliwa namaadui, kwa lengo la kuudhofisha Uislamu.
Moja wapo ya hukmu za Kiislamu zinazopigwa vita kwa wingi na wamagharibi ni Jihad.Kwa kupitia vyombo vya habari wamagharibi wamefaulu kwa kiasi kikubwa kuchafua mabongo ya wasokuwa waislamu kuchukia Waislamu na Uislamu. Kumejengeka dhana mbovu kwa watu wengi wasojua Uislamu kuwa Waislamu ndio wachangiaji wa mauaji ya watu kote duniani kwani hao ni magaidi.Wamagharibi wameitungia jihadi jina jengine ‘vita vitakatifu’[Holy war] kueneza urongo dhidi yake na kuonyesha kwamba waislamu ndio wawauaji wakubwa na wao ndio chanzo kikubwa cha ukosefu wa usalama duniani. Kampeni hii imewafanya Waislamu wakiwemo mashekh kuanza kujisafisha kwenye vyombo vya habari kwa kupindisha hukmu ya Jihad na wengine kuanza kuomba samahani serikali hususan kunapotokea mashambulizi.Licha ya kuwa mashambulizi mengi yaitwayo ya kigaidi hutekelezwa na serikali kisha kusingiziwa Waislamu,wengi ya Waislamu wameshindwa kabisa kufafanua suala hili kwa sura yake halisi bali wamekuwa wakionekana kutupiana lawama.Hii ina maana kuwa tayari baadhi ya Waislamu wamekubali kuwa wao ni magaidi. 
Jihadi iliwajenga Waislamu moyo wa ushujaa na ujasiri wa kutokubali kuonewa au kudhulumiwa. Walijitolea kwa hali na mali kuutetea Uislamu, kila pale zilipojitokeza dalili za kutaka kuhujumiwa. Watetezi hao ndo walioitwa Mujahidina. Cheo cha Mujahidina kilikuwa kina daraja bora, na kila Muislamu alitamani akifikie. Mtume (saw) alipoulizwa, "Mtu gani ni bora?" Alijibu, "ni muumini anayefanya juhudi katika njia ya Allah, kwa mali yake na nafsi yake", yaani "Mujahid".
Jihad ikawa ni tishio kwa maadui. Waligundua kuwa madamu Waislamu watadumu na moyo wa kujitolea kwa ajili ya jihadi, basi hawatashindwa na lolote. Wakaona hakuna njia ya kuudhofisha Uislamu na Waislamu wenyewe, isipokuwa ni kuifanya jihadi iwe ni chukizo nyoyoni mwa watu. Wakaanza tafsiri potofu ya neno hilo. Wakalitafsiri neno jihadi kwa maana ya vita vitakatifu. Wamefanya hivyo ili ionekane kuwa Uislamu ni dini ya vita na mauaji. Wakaufanya Uislamu ni dini iliyotumia nguvu kuwalazimisha watu waikubali. Wakachora katika akili za watu picha inayoonyesha kuwa jihadi ni vita vya kusaka makafiri na kuwaua. Na wanaposema Mujahidina hukusudiwa jeshi la watu waliovaa kanzu, waliopiga vilemba vichwani, waliofuga madevu mengi mengi, wanaofananafanana na Waarabu, au ‘Wamanga", kama walivyozoea kuwaita walioshika panga mikononi, wanaozunguka huku na kule kuua makafiri. Ndiyo maana hawaoni aibu kupaza sauti zao na kuutangazia ulimwengu, kuwa kuna makontena bandarini yanayotaka kutumiwa na Mujahidina kuchinjia makafiri. Na vyombo vya habari navyo bila ya kutafiti na kupata ithbati, tayari wanazishabikia habari hizo na kuzieneza.
Kwa vile panga na majambia si silaha tena katika zama hizi, basi sasa Mujahidina, moja kwa moja wanahusishwa na ulipuaji mabomu. Kila linapolipuka bomu wa mwanzo kushutumiwa huwa ni Mujahidina. Imejengwa dhana kuwa Waislamu tu ndio wakorofi wa kutega mabomu. Asiye Muislamu huonekana ni mstaarabu, na ni mtu mwenye upendo, hawezi kushiriki katika vitendo vya ugaidi hata kama ushahidi utaunyooshea kidole! Tokea lini ugaidi ukawa una dini, kabila au rangi?
Uislamu si dini ya mabavu. Uislamu unajali zaidi hoja na siyo nguvu. Unamtaka mwanadamu atumie akili yake katika kumtambua Muumba wake. Ndiyo ukaona Qur’an Tukufu haimlazimishi mtu kumkubali Mwenyezi Mungu bali inamtaka binadamu atumie akili kuzingatia Qur’an inasema: "Je! Hwawatazamia ngamia jinsi walivyoumbwa? Na mbingu jinsi zilivyoinuliwa. Na milima jinsi ilivyothubutishwa. Na ardhi jinsi ilivyotandazwa?" (Al- Ghashiyah 88:17-20).
Mwenyezi Mungu (sw) anawataka wanaadamu watazame umbo la ngamia, mbingu, majabali na ardhi, kisha watumie akili zao kupima ili waone kama vyote hivyo vimekuja vyenyewe hivi hivi au yuko aliyeviumba? Kisha Mwenyezi Mungu (sw) akamwambia Mtume wake, "Basi kumbusha, hakika wewe ni mkumbushaji (tu). Wewe si mwenye kuwatenza nguvu’. (Al-Ghashiyah 88:21-22)
Utaona Uislamu umeilenga zaidi akili ya mwanadamu. Mwanadamu amekuwa ni kiumbe bora kuliko mnyama kwa sababu ya akili aliyo nayo. Binadamu asiye na akili hatafautiani na mnyama. Mwenye akili hupima kila analoambiwa. Akiliona linakubaliana na akili analikubali na akigundua halikubaliani na akili, basi naye hulikataa. Na Uislamu ndivyo ulivyo. Hoja zake zinachuana na akili ya binadamu. Kama akili inakataa kukubali kuwa 1 + 1 + 1 ni 3, kwanini basi akili itaabishwe kwa kupewa jawabu isiyoridhia na ya uwongo?
Ukweli na uwazi umekuwa ndiyo silaha kubwa ya Uislamu. Na kwa silaha hiyo Uislamu umeweza kuwateka wengi sana. Baada ya kuonekana wengi wanasalimu amri mbele ya hoja za kweli za Uislamu wengine hawakuweza kulivulia hilo litendeke mbele ya macho yao.
Ndiyo wakavumbua kila aina ya kisingizio. Ati wahubiri wa Kiislamu wanazikashifu dini nyingine. Sheria ya nchi inamtaka mwenye kukashifiwa aende mbele ya vyombo vya sheria kushitaki. Lakini mpaka hivi leo, bado haijajitokeza madhehebu yoyote ya kidini kushitaki kuwa imekashifiwa, jambo ambalo linathibitisha kuwa hapana anayekashifiwa.
Na vipi Muislamu atakashifu dini nyingine na wakati Uislamu wenyewe unakataza kufanya hivyo.
Qur’an Tukufu inasema, "Wala msiwatukane wale ambao wanaabudu, kinyume cha Mwenyezi Mungu, wasije wakamtukana Mwenyezi Mungu kwa jeuri zao bila kujua". (Al An-Am 6:108). Na Mwenyezi Mungu (sw) alimwagiza Mtume wake kwa kumwambia, "Waite (watu) katika njia ya Mola wako kwa hekima na mawaidha mema, na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora (siyo kwa kuwatukana wao au kutukana dini zao)". (An Nahl 16:125).
Mtume (saw) akafuata maagizo ya Mola wake. Kwa miaka 13 mfululizo aliwalingania watu wa Makka kwa maneno mema, hekima na busara. Katu hakuwatukana wala kutumia nguvu. Kinyume chake yeye na wafuasi wake ndio waliokuwa wakitukanwa, kunyanyaswa na kuteswa.
Na kila mara Mwenyezi Mungu akimwambia, "Basi wasamehe na uwaambie (maneno ya) salama (labda mwisho wake watatambua). Hivi karibuni watajua". (Az-Zukhruf 43:89).
Na pale alipofanyiwa uovu aliambiwa, "Ondosha mabaya (unayofanyiwa) kwa (kulipa) mema". (Al Muuminun 23:96). Hatimaye ilibidi Mtume (saw) na masahaba wake wakimbie Makka kusalimisha maisha yao.
Huenda mwulizaji akauliza itakuwaje isemwe kuwa Uislamu ni dini ya amani, na jihadi siyo vita na kumbe Waislamu walipigana vita vya jihadi? Swali hili ni zuri sana. Vita hupiganwa kwa malengo mawili makuu. Aidha kwa kupigania maslahi ya kidunia, kama kutaka kuziteka na kuzitawala nchi nyingine, kupata mali ghafi au masoko ya kuuzia bidhaa, au pia vita vinaweza kupiganwa kwa ajili ya kujilinda na mashambulizi ya adui.
Kwa vyovyote vile vita hivyo viwili havifanani. Vile vya aina ya kwanza ni vya uchokozi na vile vya pili ni vya kujihami. Uislamu unaviita vile vita vya uchokozi "Harbun" na vile vya kujihami "Jihadun".
Ilitarajiwa Waislamu wafanye nini baada ya kudhulumiwa uhuru wa kuabudu na kufukuzwa katika nchi yao? Iisitoshe na hata walipokimbilia Madina kama wakimbizi na kupewa hifadhi ya kisiasa huko bado waliandamwa na maadui na kushambuliwa.
Bila shaka hiyo ni jeuri iliyopindukia na hakuna atakayeivumilia. Ndipo hapo Mwenyezi Mungu (sw) akawapa Waislamu ruhusa ya kupigana. Ruhusa ya kwanza waliyopewa ilikuwa "Wameruhusiwa (kupigana) wale wanaopigwa, kwa sababu wamedhulumiwa. Na kwa yakini Mwenyezi Mungu ni muweza wa kuwasaidia ambao wametolewa majumbani mwao pasipo haki ila kwa sababu wanasema ‘Mola wetu ni Allah’ (Al Hajj 22:39-40)
Huo ukawa ndio mwanzo wa vita vya jihadi. Lakini msisitizo mkubwa waliowekewa ulikuwa wasipigane vita vya uvamizi bali vita vya kujihami. Na shahidi wa haya ni ile kauli ya Allah (sw) inayosema, "Na piganeni katika njia ya Mwenyezi Mungu na wale wanaokupigeni, wala msipindukie mipaka (mkawapiga wasiowapigeni). Kwani Mwenyezi Mungu hawapendi warukao mipaka" (Al Baqarah 2:190).
Ukichunguza utaona kila lnapotajwa neno jihadi katika Qur’an Tukufu au katika hadithi za Mtume (saw) basi huongezwa Fiy Sabilil Lahi. Maana yake jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu. Hii ni kwa ajili ya kuonyesha kuwa si lazima jihadi kila siku iwe ina maana ya vita.
Neno juhudi pamoja na kustahamili mashaka na taabu katika kufikia jihadi ni kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu kwa kustahili kila aina ya misukosuko inayoweza kumfika mtu. 

  

MWEZI WA MUHARRAAM NA UZUSHI

بسم الله الرحمن الرحيم MASHIA NA BIDAA ZA MWEZI WA MUHARRAMU. Mwezi wa Muharramu ni miongoni mwa miezi mitukufu kwa mujibu wa mafundis...